Thursday, December 29, 2011

KRISMASI - CHANZO CHAKE

Leo nimeona ni vema nitoe majibu ya swali lililoulizwa na wakristo wengi juu ya chanzo cha sikukuu ya Krismas ya tarehe 25 Desemba.
Swali:
Ni nini Chanzo cha sikukuu ya Krismass ya tarehe 25 Desemba? Je ni kweli Yesu alizaliwa tarehe hiyo?
Jibu:
Wakristo wengi wanaamini kuwa Yesu hakuzaliwa tarehe 25 December, kwa sababu Mariamu alipata uja uzito kati ya Mwezi wa sita (Juni) mwishoni – Hivyo kama kawaida ya binadamu, uja uzito unachukuwa miezi tisa ili mtoto azaliwe, hivyo ni wazi Yesu alizaliwa majira ya mwezi wa Februali. Ila hakuna Andiko la Biblia wala Historia iliyoweka kumbukumbu ya tarehe ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Kwenye Biblia tunaikuta tarehe 25 December, kuwa ni sikukuu iliyokuwa inasherehekewa na wapagani wa Babeli ambako Waisraeli walichukuliwa mateka. Hivyo sikukuu ya 25 Desemba ilikuweko kabla ya Kuzaliwa Yesu, na ilikuwa sikukuu ya wapagani wa Babebli wakisherehekea kuzaliwa kwa Mtoto wa Mungu JUA aliyeitwa TAMUZ.

Kulikuwa na Mfalme wa babeli aliyeitwa Nimrodi, na mke wake Nimrodi ambaye pia aliitwa Malkia wa Mfalme jina lake aliitwa Semiramis, baada ya Mfalme Nimrudi kufariki, Mke wa mfalme akabeba mamba nje ya Ndoa. Ili kuficha kitendo hicho cha mke wa mfalme kubeba mimba wakati mume wake amefariki, akatunga UONGO kuwa Mume wake HAKUFA ila alibadilika kuwa Jua (SUN), hivyo mionzi ya Jua wanayoiona ndiyo iliyomdunga Mimba. Wababeli kwa kuwa walikuwa waabudu mizimu waliamini Uongo huo na kuanza Kuliheshimu Jua (SUN) kama Mungu wao.

Usiku wa kuamkia Tarehe 25 Desemba, Semiramis akazaa Mtoto aliyemwita TAMUZ, ambaye baba yake ni Mungu Jua. Imani yao ilienda mbali zaidi hadi kuamini kuwa tendo la Semiramisi kuzaa na Mungu jua yeye pia ni Mungu Mke na Mtoto wao Tamuz akaitwa Mungwa Mwana. Kuanzia kipindi hicho wapagani wa Babeli tarehe 25 mwezi wa 12, waliweka sherehe kubwa ya kuzaliwa kwa Mungu Mwana Tamuz.

Biblia inatoa maelezo juu ya jambo hilo la kufanya sherehe ambayo mfalme aliitumia kufungua baadhi wafungwa, kama msamaha wakati wa sikukuu - Yeremia 52:31Hata ikawa, katika mwaka wa thelathini na saba wa kuhamishwa kwake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kumi na mbili, siku ya ishirini na tano ya mwezi, Evil-Merodaki, mfalme wa Babeli, katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, akamwinua kichwa chake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani.”

Nabii Yeremia aliandika kitabu hicho zamani kabla ya Yesu kuzaliwa, taifa la babeli lilikuwa na Desturi ya kuweka huru wafungwa katika siku hii ya Kuzaliwa kwa Tamuz tarehe 25 Desemba. Enzi hizo haikuwa inaitwa Krismass huenda iliitwa Tamuz–Mass.

Baada ya Yesu kuzaliwa, hapakuwa na Sikukuu ya Krismass hata mitume hawakuwahi kusherehekea sikukuu hii, bali tunaona baada ya miaka mingi kupita karibia zaidi ya miaka 300 Mfalme Constatino wa Dola ya Kirumi aliyekuwa anaabudu JUA alimua kuwa Mkristo, lakini hakutaka kuacha Desturi za kuifanyia sherehe miungu yake. Hivyo akaamuru sherehe ya kuzaliwa Mungu Mwana Tamuz iendelee kusherehekewa ila wakristo waambiwe kuwa ni siku ya kuzaliwa Yesu Kristo. Kulingana na kitabu cha Historia ya kanisa la RC, ambacho hata mimi ninacho, kinachoitwa  “The Compact History of Roma cathoric church” kinaeleza juu ya tangazo la Mfalme Constantino kwa wakristo kuanza kuadhimisha  sikukuu za kipagani ikiwemo Ibada ya JUA ya siku ya Kwanza (SUN-DAY) badala ya Ibada ya Siku ya SABA, historia inaeleza kuwa alitoa maagizo hayo akiwa bado mpagani (Kabla ya kubatizwa), tangazo hilo lilitolewa mwaka 325AD.

Historia inasema, ilikuwa ni mwaka 336AD, ndipo kanisa lilipoamua kwamba, badala ya kuwa na sikukuu ya kipagani mjini Rome iliyojulikana kama “Natalis Solis Invincti” au The Birthday of the invincible/unconquered Sun, iliyosherekekewa tarehe 25 Desemba, sasa tarehe hiyo iwe si kwa kuzaliwa jua, bali iwe siku ya kuzaliwa mwana (son) wa Mungu – Yesu Kristo. Kwa mara ya kwanza kanisa lilikuwa linaendesha Misa tu, lakini baadaye mtindo wa sherehe za kipagani ikaingizwa hadi leo inaendelea – ikitawaliwa na Vinywaji (Vileo), Vyakula na starehe za kila namna.

MASWALI YA CHANGAMOTO:
1.    Kwa nini Mungu hakuona haja ya kuwa na siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo? Hata hakuiweka wazi tarehe na siku ya kuzaliwa kwa Yesu?
2.    Ilikuwaje Mitume na Kanisa la awali hawakuwa na wazo hilo la sherehe ya Krismasi?
3.     Kwanini wakristo walazimishwe kusherehekea sikukuu ya kuzaliwa Yesu katika tarehe ya Kuzaliwa Mwana wa Mungu JUA? Na mfalme ambaye wala hakuwa Mkristo wakati huo?
4.     Kwa nini wakristo wasiweke Tarehe ya kwao ambayo inaendana  na mwezi hata kama Tarehe haijulikani? Make miezi tisa kutoka June ni February / March.

MUNGU AWABARIKI WOTE MNAPOENDELEA KUTAFAKARI JUU YA UKWELI HUU UNAOTUSAIDIA  KUKUA KIROHO.

Ev. Eliezer Mwangosi
0755808077 & 0652571733
Kumbuka kuwapelekea wengine – Pia ukiwa na swali zaidi unaweza kuuliza

Wednesday, December 28, 2011

KIFO CHA MWANADAMU

MARA BAADA YA KIFO KUNA NINI ?

Kuna mafundisho mengi tofauti juu ya Mtu anapokufa, wengine wanasema anaenda kuzimu, wengine jehanamu, wengine peponi, wengine haendi kokote. Je Mungu anasemaje ?,  jibu la kweli tunalipata kutoka katika Neno la Mungu kama lilivyochambuliwa kwenye vipengele vifuatavyo.

(1)  MTU  AU  NAFSI HAI 

Mtu au Nafsi HAI ni muungano wa vitu viwili  MAVUMBI na PUMZI YA MUNGU, ( Mwanzo 2:7,  Ezekiel 18:4   Isaya 53:12 ), Au  NAFSI HAI = MAVUMBI + PUMZI YA MUNGU. Hivyo, vitu hivi viwili vikitengana hamna nafsi HAI na ndicho huitwa kifo, mtu anakuwa kuzimu.

(2) KUZIMU KUNA NINI ?

Maandiko yanasema KUZIMU ni sehemu penye ukimya, Mtu aliyekufa au aliyekuzimu hawi na Ufahamu, hivyo hajui lolote juu Mbinguni na Duniani. ( Mwanzo 3:19, Mhubiri 3:18-20, Mhubiri 9:5-6, Zaburi 104:29 ). Pumzi inayomrudia Mungu sio nafsi hai, hivyo inakuwa sawasawa tu na kabla ya mtu hajazaliwa au kuumbwa.

(3)  WAKRISTO HALISI HUKIITA KIFO KUWA NI NINI ?

Neno la Mungu linasema kifo ni sawa na USINGIZI, Daudi alikiita kifo kuwa ni USINGIZI WA MAUTI. Kama mtu asivyojua lolote akiwa usingizini ndivyo Marehemu anavyokuwa kabulini hadi kristo atakapokuja. ( Daniel 12:2, Yohana 11:11, Mathayo 27:52, 1Thesalonike4:13, Ayubu 17:13, Luka 8:52-53, Zaburi 13:3, 1Korintho 15:20-23 ).

(4)  KUNA UHUSIANO WOWOTE KATI YA WALIOKUFA NA MUNGU ?

Mungu hana uhusiano wowote na waliokufa, kwa sababu hawana kumbukumbu lolote, Pia Kristo alisema Mungu sio wa waliokufa. ( Mathayo22:32,  Zaburi 146:1-4 ). Hivyo watakatifu wote waliokufa hawako Mbinguni wamelala kabulini.

(4)  NI LINI WATAKATIFU WALIOKUFA WATAONANA NA MUNGU ?

Mbinguni au Peponi wanaenda watu hai au ( NAFSI HAI) wakivishwa miili ya Mbinguni ( Mfano: Eliya, Henoko, Kristo  nk. ), Kristo kama alivyotuahidi atakuja kutuchukua pamoja na waliokufa atakapokuja mara ya pili. Tutarudishiwa Pumzi na kuwa hai tena, ndipo tutavishwa miili ya mbiguni na kuanza safari ya kwenda kwa Baba yetu Mbinguni. ( Yohana 5:28-29, 1Thesalonike 4:15-17, Yohana 14:1-3, 1Korintho 15:51-52, Ayubu 14:12, Matendo 24:15, Matendo 2:34 ). Yesu mwenyewe alipokufa msalabani na kuzikwa hakuenda mbinguni hadi alipofufuka ( Yohana 20:17 )

(5)  LINI WAOVU WATAINGIA JEHANAMU ?

Waovu wataingia Jehanamu baada ya Kristo kupitisha hukumu, Ni ahadi ya kristo pia kuja siku ya mwisho kuuhukumu ulimwengu na kutoa adhabu ya Moto. Waovu watafufuliwa katika ufufuo wa pili, wote watakuwa hai na kudhihirishiwa matendo yao yote, ndipo MOTO utawashwa kwa ajili yao. ( Ufunuo 6:14-17,  20:13-15, 22:12,  Mathayo 16:27,  2Petro3:7-10, Isaya 25:9, Yohana 5:28-29, Mathayo 25:31-41, Malaki 4:1, Rumi 2:5-6 ).

Viongozi wa dini wanaofundisha kuwa Mtu akifa hapohapo anaenda Jehanammu (Motoni) au Peponi (Mbinguni) ni lazima tuwaangalie sana huenda kwa kujua au kutokujua wanatumiwa na yule adui kwa hila kuvuruga ukweli halisi juu ya mpango wa Mungu Kuuhukumu ulimwengu kwa haki kama Injili inavyosema.




MAFUNGU YA BIBLIA YANAYOTUMIWA KUPOTOSHA UKWELI

WAEBRANIA 9:27.
Kama tulivyosoma hapo juu baada ya Kifo hakuna kinachoendelea, yaani mtu hana nafasi tena ya kuamua kufanya mema au mabaya. Kilichoandikwa kitabuni mbinguni dakika ya mwisho ya kukata Roho, ndicho kinapelekwa hukumuni siku ya mwisho Kristo atakapokuja. Mtu akifa rekodi za matendo yake zinafungwa tayari kwa hukumu. Pia neno la Mungu linasema hukumu kwa waliokufa imeshaanza, hii inaitwa hukumu ya upelelezi ambapo vitabu vya kumbukumbu kwa waliokufa vinapitiwa mmoja baada mwingine hadi siku ya Mwisho.

LUKA 23:39-43.
Hapa Kristo alikuwa anamhakikishia mhalifu kuwa watakuwa wote peponi, Neno halijasema "LEO HII" Kristo amesema "LEO HIVI".  Hapo kuna makosa ya uchapaji na tafsiri kutoka lugha ya awali ya kigiriki,  alama ya koma (,) kwa kiswahili sahihi haijawa mahali pake. Hata hivyo kama tulivyosoma Kristo alithibitisha kuwa hakuenda Mbinguni (Peponi) alipokufa ( Yohana 20:17, Yohana 14:1-3 ). Pia ukumbuke kuwa Mungu sio kigeugeu na neno lake halipingani.

LUKA 16:19-28.
Mfano huu wa Tajiri na Maskini Lazaro, umekuwa ni kigezo kikubwa cha Shetani kutumia kuwavuruga watu washindwe kuielewa Injili na ahadi za Kristo. Kabla ya kutoa maelezo juu ya mfano huo soma na kutafakari mifano mingine iliyotolewa na Kristo ( mfano: Luka 16:1-15 ) Je unaweza kusema "Kristo alihalalisha mali ya Udhalimu ? ", Mifano iliyotolewa kwenye Biblia, kabla hatujaichukuwa kama mafundisho, ni lazima tuangalie vitu vufuatavyo : Mfano ulitolewa na nani, Kwa watu wa aina au hali au Tabia gani, Dhumuni au Fundisho maalumu la mfano, na Je biblia nzima inasemaje juu ya Fundisho hilo.

Katika mfano huo Fundisho au Dhumuni lilikuwa juu ya hali halisi ya Matajiri wenye Ubinafsi na Maskini, itakavyokuwa wakati Kristo atakapokuwa akimlipa kila mtu mshahara wake.  Kristo hakuwa na maana kuwa mtu akifa anakwenda Peponi au Jehanamu halafu wanakuwa wanawasiliana. Shetani anajua kuchanganya ukweli na uongo lakini kwa kuichambua biblia nzima kwa msaada wa Roho mtakatifu, siri zote za muovu zinafichuliwa. Watu wengi leo wamechanganyikiwa hadi wanasema biblia inajipinga.

MAFANIKIO YA SHETANI KUPITIA SOMO ZIMA LA WAFU
[A]
Shetani amefanikiwa kueneza uongo wake aliousema kwa mama yetu EVA katika Bustani ya Edeni. Mungu alisema "hakika mtakufa", Shetani alisema "hakika hamtakufa". Hata hivyo Mungu kwa njia ya manabii, Kristo na Mitume amezidi kuthibitisha kuwa Binadamu sharti afe, Kufa ni Amri tangia Edeni. Na shetani anaendeleze uongo kuwa Mtu hafi ila anabadilishwa mwili na kuwa na nafsi hai.
[B]
Amewaingiza wengi kwenye Ibada za Umizimu bila kujua. Kuomba, Kuongea na Wafu na kuwaombea wafu ni Ibada za Umizimu, Kwa kuamini kuwa Wafu wako mbinguni, Shetani anajigeuza na kuja kwa sura za watakatifu waliokufa na kuwaagiza watu wamwabudu Mungu kwa njia ambazo zingine ni kinyume na Maandiko. Ibada ya Sanamu, Lozari na sadaka ya wafu walioko pagatori ni baadhi ya mafundisho yaliyoingizwa kanisani kwa hila ya mwovu na wengi hawajui. Kuomba au kuwaombea Wafu Ni machukizo kwa Bwana ( Kumbukumbu la torati 18:9-12 ).
[C]
Amefanikiwa kueneza Imani ya Pagatori, ambayo amewafanya mamilioni  ya watu wapotee, kwa kutojiandaa wakiwa Hai, wakitegemea kuja Kuombewa na kutolewa sadaka ya msamaha na ndugu zao walio hai  ili watoke Pagatori na kwenda peponi.
[D]
Amewafanya wengi wachanganyikiwe wasielewe sawasawa Ahadi za Kristo juu ya Kurudi mara ya pili kuja kuuhukumu ulimwengu, na Injili kuhusu Kiama imevurugwa. Pia amewaminisha wengi kuwa Mungu si wa HAKI kwani anawapeleka Jehanamu kabla ya, Hukumu na wenye Mapesa wanaweza kumlipa wakasamehewa wakiwa pagatori, hivyo kumfanya Mungu kuwa anaupendeleo.

Ndugu yangu inakupasa uchague leo kuwa katika wokovu wa kweli au wokovu ambao Kristo aliuita wa watu
 wapumbavu, yaani wale wanaomkiri Kristo kuwa mwokozi wao kwa midomo tu ila wanakataa kutii Neno lake.

Yesu anakuita kwa Upole na kukutahadharisha, Fanya uamuzi sasa.

[ Mathayo 7:24-27  ,   Ufunuo 18:4-5 ]

Tuesday, December 6, 2011

SHERIA ZILIZOISHIA MSALABANI

Somo hili ni la maana sana kujifunza kwa ajili ya wokovu wetu, shetani amejaribu kulitumia somo hili kama mtego wa kuwanasa watu hasa wale ambao hawana muda wa kukaa na kutafakari kwa undani neon la Mungu, wakitegemea maelezo ya viongozi wao wa dini au madhehebu.
Kuna mafungu mengi katika Biblia yanayoeleza kuwa kuna sheria zilizoishia msalabani, ambazo zilikuwa kivuli cha mambo yaliyokuwa yanatazamiwa. Mtume Paulo anasema Sheria ikishikwa sasa Kristo si Mwokozi wetu kwa sababu tunategemea sheria iliyokufa [Wagalatia 5:4-6, 4:1-11]. Hivyo wengi hawaelewi, na kuna maswali mengi kuhusu sheria zilizokufa baada ya Kristo kufa msalabani, kwa sababu Biblia kwa upande mwingine inasisitiza juu ya ulazima wa kutii na kushika Amri za Mungu kwa yeyote aliyeokolewa. Soma: 1Yohana2:4 “Asemaye nimemjua wala hashiki Amri ni muongo wala kweli haimo ndani yake”, Mithali 28:9, Ufunuo 14:12, Marko 7:6-8, Mathayo 5:17-19   n.k..

Katika Biblia Sheria zimegawanywa katika makundi makuu mawili na zinaitwa Sheria za Mungu na Sheria za Musa. Kabla hatujaelezea ni kwa namna gani zinategemeana, yafuatayo ni maelezo yanayotoa tofauti kati ya hayo makundi mawili.


SHERIA YA MUNGU
1.  Iliandikwa na Mungu Mwenyewe 
     (Kutoka 31:18)
SHERIA ZA MUSA [TORATI]
1.  Iliandikwa na Musa
     (Kutoka 31:9)
2.  Iliandikwa juu ya Mawe
     (Kumbukumbu 10:1-4, 9:10 )
2.  Iliandikwa ndani ya Gombo au Kitabu
     (Kumbukumbu 31:24)
3.   Ilitunzwa ndani ya Sanduku la Agano
      (Kumbukumbu 10:5)
3.  Ilitunzwa Nje ya sanduku la Agano
     (Kumbukumbu 31:26)
4.  Huitwa Sheria ya Mungu
     (Zaburi 1:2, 11:1)
4   Huitwa Sheria ya Musa
     (Malaki 4:4, Mathayo 15:5)
5.  Ni za Milele na ni Kamilifu
     (Zaburi 111:7-8, Mathayo 5:17-19,  Zaburi 19:7)
5.  Baadhi ziliondolewa na sio kamilifu
     (Ebrania 9:10-11, 7:1, Efeso 2:15)
6.  Ni Takatifu, ya Haki na Njema
     (Warumi 7:12)
6.  Baadhi zilikuwa kivuli cha Kifo cha Yesu Kristo
     (Ebrania 10:1, 7:12) – Iliishia msalabani
7.  Jumla ziko kumi
     (Kumbukumbu 4:12-13)
7.  Ziko nyingi (Huitwa chuo)
      (Kumbukumbu 31:24-26, 2Nyakati 35:12)
8.  Ndiyo Jumla na Muhtasali wa Mapenzi ya Mungu,  Ndiyo
     huonyesha Dhambi ni nini.
     (Mhubiri 12:13, Rumi 2:13, Yakobo 2:10:12,
      Rumi 7:7, 3:20)

8.   Kwa wakati wake zilimsaidia mtu kuhesabiwa haki  na
       kuwafanya wengi waogope kutenda dhambi au kuvunja
      Amri za Mungu. Mfano. Sheria za Kafara.



Kiini cha kuwepo Sheria za Musa, na Kristo kuja kutufia msalabani ni Dhambi (Uasi wa Sheria za Mungu).  Amri kumi zikiondolewa hakutakuwa na Dhambi, hivyo hakutakuwa na hukumu, na hatimaye hakutakuwa na haja ya kuwepo Mwokozi, na tendo la msalaba litakuwa bure. Shetani ametumia mbinu ya kuzichanganya sheria hizi mbili na  amefaulu kuwateka mamilioni ya watu wa Mungu bila ya wao kujua. Sheria au Amri za Mungu ndicho kipimo cha wokovu na utiifu wetu kwa Mungu, wala haziwezi kubadilika kwa maana YEYE NI MKAMILIFU NA SHERIA ZAKE NI KAMILIFU WALA HANA KIGEUGEU [Isaya 8:20, Mithali 28:9, Yohana 14:15, 15:10, 8:29].

Amri za Mungu kama zilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu mwenyewe katika mbao mbili za mawe, ndizo jumla ya mapenzi ya Mungu, na ndicho kioo kinachotuonyesha kuwa tuko safi au wachafu. Shetani leo amefaulu kuwaongoza wengi kuzichukia Sheria za Mungu wala hawataki kuzisikia. Amri za Mungu zinapatikana katika Kutoka 20:1-17,  Hebu chukua Biblia yako na usome  mistari hiyo, kasha linganisha na jinsi ulivyofundishwa Amri za Mungu au linganisha jinsi zilivyoandikwa kwenye vitabu vya mafundisho. Mfano: Katekisimo ya Kanisa lako. Kama utakuta kuna tofauti basi fanya maamuzi ya kufuata Neno la Mungu kama Yesu alivyotoa wito katika Injili ya  Marko 7:6-8. Kuendelea kushika Mapokeo au mafundisho ya wanadamu na kuziacha Amri za Mungu ni kuchagua kupotea milele, na Ibada yako itakuwa ya Bure kama Kristo alivyotoa tahadhari.

MAELEZO JUU YA SHERIA ZILIZOISHIA MSALABANI

1. SHERIA ZA KUTOA KAFARA [ UPATANISHO AU ONDOLEO LA DHAMBI
Tangu mwanzo Mungu alimwambia mwanadamu kuwa akiasi maagizo hakika atakufa Mwanzo 2:16-17, hata hivyo kwa rehema zake akaandaa mpango wa wokovu kwa Mwanadamu aliyeanguka dhambini, mpango ulikuwa ni kumtoa mwane Yesu Kristo afe badala ya Mtu aliyeasi. Kabla ya Kristo kufa msalabani Mungu aliweka taratibu zingine ambazo zilikuwa badala ya Kafara halisi ya Kristo. Mwanzoni alitoa Sheria ya Tohara na baadaye Mungu aliruhusu Wanyama watolewe kafara ikiwa ni kivuli cha kafara halisi ya Kristo. (Walawi 4:27-29, 17:11, 16:5-30, Ebrania 9:7). Siku maalumu za kufanya huduma hizo, ziliitwa Sabato au Pumziko takatifu kwa ajili ya Upatanisho (Walawi 23:26-32, 25:8-10), pia kulikuwa na sikukuu za miandamo ya miezi zilizofuatia siku hizo za Upatanisho (Hosea 2:11).

Sikukuu hizo za upatanisho pamoja na Kafara vilikuwa kivuli cha Kafara halisi ya Kristo, hivyo vilikoma baada tu Yesu Kristo kufa pale Msalabani. Waebrania 9:25-26. Baada ya hapo wote tunaokolewa kwa neema ya Kristo iliyotokana na Kafara yake iliyotolewa mara moja pale Kalvari.

2. SHERIA ZA KIJAMII
Sheria hizi zinaitwa za kijamii kwa sababu zilitumika kulinda amani katika jamii, na kuwafanya watu waogope kufanya uovu (Watii sheria za Mungu).  Adhabu kali zilitolewa kwa yeyote anayevunja Amri za Mungu  Mfano: Kuwapiga mawe wazinzi hadi kufa. Watu waliogopa kutenda uovu kwa sababu ya adhabu sio kwamba walimheshimu Mungu ndani ya mioyo yao.

Baada ya Kristo kufa msalabani, wale wote wanaofungua mioyo yao na kumpokea Yesu Kristo kwa Imani, wanapokea Uweza wa kushinda dhambi.  Uweza wa Mungu hujenga asili ya kuchukia dhambi ndani ya Moyo wa Mwanadamu. Hivyo sheria za kumuogopesha mtu asifanye dhambi wakati Moyo wake unapenda au kutamani dhambi hazina kazi. Hiki ndicho kipimo cha Mkristo aliyezaliwa mara ya Pili. Yeyote mwenye Moyo wa Kutamani dhambi, hata kama inashindikana kutekelezwa, Mungu anamhesabia dhambi Matahayo 5:27-28, kwa sababu ni wazi mtawala wa Moyo ni Shetani sio Roho Mtakatifu.

3. SHERIA ZA AFYA
Ni sheria ambazo Mungu alizitoa kwa ajili ya kulinda Afya za watoto wake, alitoa maelekezo juu ya Vyakula vinavyofaa kuliwa na visivyofaa, hii ilikuwa kwa ajili ya Afya. Kwa maelezo zaidi juu ya somo hili la AFYA, nimeandaa somo maalumu linaloezea uhusiano uliopo juu ya Afya zetu na Wokovu.

WOKOVU NA SHERIA
Fundisho la Biblia kuhusu sheria zote mbili juu ya wokovu ni kama ifuatavyo:

1.    Wale wote waliompokea Kristo hawako chini ya Sheria za Makafara, wako huru Kabisa.

2.    Baada ya Kristo kuja, hakuna sheria za adhabu za kijamii – mf. Kupiga mawe wazinzi n.k.

3.   Sheria za Mungu [Amri Kumi] hazimuokoi Mtu, zenyewe zipo kama kioo kinachoonyesha uchafu lakini haziwezi kukusafisha, ili uchafu utoke ni lazima uchukue Maji unawe. Maji ni Damu ya Kristo ambayo kwa Imani tunatakaswa kwayo. Kutunza au kutii sheria ni matokeo ya kuokolewa, ni yule tu aliye chini ya Neema ya Kristo, ndiye anayeweza kutii mapenzi ya Mungu.

NB: Hatuhesabiwi haki kwa sababu tunashika Sheria za Mungu, bali tunahesabiwa haki kwa sababu NEEMA YA YESU KRISTO imetupatia ushindi wa Dhambi na kutufanya tuwe safi pasipo mawaa mbele za Mungu. Kujitahidi kutii Amri za Mungu kwa Nguvu zetu, kutaka kuhesabiwa haki kwa matendo ya Sheria, kitu ambacho hakiwezekani.

 Kitu cha kushangaza ni pale wengi wanadai wameokolewa huku wakiendelea kuvunja au kutotii baadhi ya Amri za Mungu kwa kusingizia kuwa chini ya Neema. Tito 2:11-12, Inatueleza kazi ya neema, Yesu hakufa msalabani ili baadhi ya dhambi zihalalishwe, alikuja ili kile kilichoshindikana kwa mwili kiwezekane kwa uwezo wa Roho mtakatifu, kwa ajili ya kutukamilisha tuonekane bila mawaa mbele za Mungu wakati wa Hukumu. Na kama tunakiri kuwepo kwa hukumu ya haki, basi ni lazima tujue kuwa kuna vigezo ambavyo vitatumika kuhukumu ambavyo Mungu anasema ni Amri zake.
Na: Ev.  Eliezer  Mwangosi