Sunday, March 4, 2012

MASWALI JUU YA TOFAUTI ZA IMANI

UTATA KATIKA TOFAUTI ZA DINI NA MADHEHEBU
1.      Kwa nini kuna Migawanyiko ya dini na Madhebu? Je ni Mpango wa mungu?
Sio mpango wa Mungu neno linasema “Bwana mmoja, Imani moja, Ubatizo mmoja” Efeso 4:5.  Hivyo ni kutimiza unabii wa biblia unaosema; “Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe, watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wanamasikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za Uongo” 2Timotheo 4:3-4.

Na Yesu alitoa tahadhari akisema “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali … Si kila mtu aniambiaye, Bwana , Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu” Mathayo 7:15-23, Mathayo 24:24-25.

Migawanyiko hii ilianza kutokea, mara tu baada ya Kanisa la Mitume kuhujumiwa na utawala wa Dola ya Kirumi, na kuanza kuingiza Mafundisho tofauti na biblia na kuamua kufanya marekebisho kwenye Amri za Mungu. Jambo hili lilitabiriwa na nabii Daniel “Naye atanena  maneno kinyume chake aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake aliye juu, naye ataazimu kubadiri majira na Sheria …” Danilel 7:25, Pia Isaya alionyeshwa Dunia yetu ikiingia katika laana kwa sababu ya Uasi wa Sheria “Tena Dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi Sheria, wameibadiri Amri, wamelivunja Agano la Milele” Isaya 24:4-6.

2.     Mbona kila Dhehebu au Dini wanaomba na Mungu anawasikia na kuwajbu?
Mambo yafuatayo tunatakiwa kuyafahamu Juu ya Ibada na kujibiwa Maombi:
-          Wachanga kiroho au wasiojua ukweli, wanapata Rehema ya Mungu, akiwasikia na kuwatendea sawaswa na ujuzi walionao, ili mradi waanamwamini Yesu. Yesu ataendelea kuwafunulia ukweli ili waweze kuukulia wokovu na kuwa wakamilifu.  Hivyo ukiona kuna ukweli wa biblia uliotofauti na kile unachokiamini, amua kuifuata Biblia utakuwa salama.

-          Watu waliofunuliwa ukweli lakini wakaamua, kuendelea kushika mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu, Mungu anawaacha na Adui Shetani anaaza kuwahudumia, akiwapatia kila wanachoomba. Wao watafikiri Baraka zinatoka kwa Mungu kumbe zinatoka kwa baba yao Ibilisi. Utashangaa Mtumishi ni Shoga, au mzinzi, muuza madawa la kulevya n.k. Huku ana upako wa ajabu, miujiza ya Baraka na uponyaji ndio nyumbani, tena kwa jina la Yesu. Hizo ndizo hila za shetani kwa siku za mwisho kama Yesu alivyotuonya kujihadhari.

3.      Mbona miaka na miaka Madhehebu tofauti yapo na yanaendelea kwa Mafanikio?  
Yesu hakusema atayaondoa, alisema,  siku ya mwisho mwisho ndipo atawaambia “SIKUWAJUA NINYI KAMWE ONDOKENI KWANGU”, bila kujali  kanisa au dini ina washiriki wangapi duniani, kama hawatii kweli ya Biblia watakwenda motoni.  Wengi wanaangalia wingi wa watu na kurithi Dini za wazazi hata kama wanaasi Sheria za mungu, hiyo ni HATARI.

4.     Kwani Dini au Dhehebu litampeleka Mtu Mbinguni?
Dini au Dhehebu halimpeleki mtu Mbinguni, bali kinachoangaliwa ni kwamba unafundishwa nini na unachukuwa uamuzi gani kwa kile unachofundishwa. Kila Dhehebu au Dini lina viongozi ambao ndio waalimu, siku hizi wanajiita manabii, Mitume, Ma baba watakatifu, Wachungaji n.k. Hatari nyingine ni hii, unaweza kuwa na katika kanisa linalofundisha kweli ya mungu, lakini usipoamua kuishi sawasawa na neno, vilevile utaangamia.

5.     Mungu ana mpango gani na watu waaminifu lakini hawaujui ukweli?
Historia inajirudia, kama ilivyokuwa wakati wa Nuhu, wakati wa Sodoma na Gomola, wakati wa Eliya, wakati Yohana Mbatizaji, Mungu hakufanya hukumu bila kutuma ujumbe wa Onyo na Matengenezo. Waliokubali kuachana na mapokeo ya viongozi wa Dini waliokolewa, hata sasa Mungu ametuma tena ujumbe wa Matengenezo kwa watu wote, kuanzia Viongozi hadi waumini wa Dini na Madhehebu mbali mbali. Anasema “Sauti ya mtu aliaye nyikani, itengenezeni, njia ya Bwana, yanyosheni Mapito yake” Mathayo 3:3, na pia Mungu anasema “Mcheni Mungu na kumtukuza kwa maana saa ya hukumu yake imekuja, Msujidieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemichemi za maji” Ufunuo 14:7. Na mwisho anasema “Tokeni kwake enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake” Ufunuo 18:4. Ni wakati wa kujiokoa nafsi, bila kujali wachungaji wala wazazi, kwani kila mtu atabeba furushi lake mwenyewe.

6.     Nikitaka leo kuamua kuishi maisha matakatifu nifanyeje?
-          Mwamini yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako, kubali kuwa wewe kwa nguvu zako huwezi kushinda dhambi, hivyo omba uwezo kutoka kwa Mungu wa kushinda dhambi. Ungama na tubu dhambi kwa kumaanisha kuziacha.
-          Amua kujifunza na kutii Sheria za Mungu kama zilivyoandikwa na Mungu mwenyewe, ili udumu kuwa safi kwa neema ya Yesu.
-          Jenga tabia ya kuukulia wokovu kwa Maombi, kusoma neno lake na kuhudhuria Ibada , pamoja na kuwashudua wengine juu ya Neema ya yesu Kristo inavyoweza kuokoa.

TUNAPASWA KUSIMAMA KATIKA UKWELI KABLA YA MAJINA YETU KIPITA KWENYE KITI CHA HUKUMU.

Ev. Eliezer Mwangosi

No comments:

Post a Comment