Sunday, March 4, 2012

MASWALI JUU YA NEEMA NA DHAMBI

MASWALI JUU YA NEEMA NA USHINDI WA DHAMBI
1.      Ninawezaje kuwa Mtoto wa Mungu?
Kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wako “Bali wote wliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu , ndio wale waliaminio jina lake”  Yohana 1:12, “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu”  1Yohana 3:9-10. “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu .

2.      NEEMA ni nini? Na ina kazi gani katika maisha Mtu?
Tendo la Mungu kutuokoa kutoka dhambini bure, kwa kutulipia gharama ya Mauti ya milele tuliyopaswa kulipa kutokana na kutenda Dhambi. Kwa njia ya Kifo cha Yesu pale msalabani, kila anayeamini, kutubu na  kuungama Dhambi, anapata wokovu bure. Ndani ya NEEMA kuna mambo yafuatayo: (i)Tunapata msamaha wa dhambi Bure, (ii) Tunahesabiwa haki ya kuwa watoto wa Mungu, (iii) Tunapewa uwezo wa kushinda Dhambi, kwa njia ya Roho mtakatifu.

3.      Dhambi  ni nini?
“Atendaye dhambi afanya uasi, kwa kuwa dhambi ni UASI  (juu ya Sheria za Mungu)“  1Yohana 3:4, Mtume Paulo amefafanua zaidi juu ya Kazi ya Sheria kuwa ni kuonyesha Dhambi, na pasipo sheria hakuna Dhambi au kosa. Warumi 4:15, Warumi 7:7-8. Yesu alisisitiza akisema “… Ukitaka kuingia katika Uzima, zishike AMRI” Mathayo 19:16-19, pia soma Mathayo 5:17-19, Marko 7:6-9.

4.       Dhambi ilianzia wapi?
Kwa mara ya Kwanza Dhambi (Uovu) ilianzia Mbinguni katika Moyo wa Malaika aliyekuwa anaitwa Lusifa ambaye anaitwa SHETANI.  Ezekiel 28:15 “Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako” soma pia Ezekiel 28:13-17, Isaya 14:13-14. Baada ya uovu kuingia kwa Shetani, Mungu akanfukuza mbinguni, akaanzisha vita akiungana na malaika theluthi moja waliokuwa wanamfuata. Ufunuo 12:4, 7-12.

5.      Dhambi  ilianza lini kwa mwanadamu?
Baada ya Shetani kufukuzwa mbinguni ndipo akashuka kuwadanganya Wazee wetu Adam na Hawa kuasi maagizo ya Mungu, na baadaye tunaona Mungu anamlaani Kaini kwa dhambi ya Kumuua Ndugu yake Habili, hadi tunaona Kizazi cha Nuhu Kinaangamizwa kwa Dhambi za Uasherati n.k. soma: Mwanzo 3:1-19 Anguko la Adamu, Mwanzo 4:6-11 Dhambi ya Kaini kumuua Habili, Mwanzo 6:1-8 Dhambi wakati wa nuhu.

6.      Amri za Mungu zilitolewa lini?
Wengi wanaamini Amri za Mungu zilitolewa katika mlima Sinai kupitia kwa Musa, na ndio maana wangi wanasema Amri kumi au Sheria za mungu ni kwa ajili ya Wayahudi.  Ukweli ni huu; Dambi ni UASI juu ya Mapenzi au Tabia ya Mungu,  hivyo  Amri Kumi alizopewa Musa na Mungu zilikuwa ni muhutasari wa Mapenzi yake ili kusaidia Kizazi kilichosahau Maagizo ya Mungu baada ya kukaa utumwani  Misri kwa muda mrefu bila kufanya IBADA kwa mungu wao.  Yesu alisisitiza watu Kushika Amri za Mungu, kama Mungu mwenyewe alivyoziandika:  Kutoka 20:3-17, ili tusihesabiwe kuwa waasi wa Mapenzi ya Mungu.

7.      Yesu alitoa Amri mpya ya Upendo, una uhusiano gani na Amri za Mungu?
Kwa ujumla Amri za Mungu zinawakilisha Tabia ya Mungu ambayo ni Upendo – Yaani kumpenda Mungu na Mwnadamu mwenzio. Na tabia ya Mungu haibadiliki hivyo hata Amri zake hazibadiliki, Yesu hakuja kubadili Amri bali kuzitimiliza, wayahudi walishika Amri kumi kibinadamu, sio kama tabia ya Mungu ya Upendo ilivyo. Na ndiyo maana Mungu alisema, Sheria zake zitaandikwa katika mioyo yetu kwa njia ya Roho mtakatifu - Ebrania 10:16, maana yake Tunapewa tabia ya Mungu, inayoonekana kwa matendo. Huko ndiko kuzaliwa mara ya Pili.

8.      Biblia inasema Kristo ni mwisho wa SHERIA, hii ina maana gani? Biblia inajipinga?
Ukisoma Warumi 10:4, Galatia 4:4-5, Galatia 3:23-25, Galatia 5:2-5, Kolosai 2:16-17 n.k. utaona mtume Paulo anapiga vita kuwa chini ya Sheria au Kushika Sheria, hii ina maana gani? Kwenye biblia, kuna sheria za aina nyingi, kuna AMRI kumi ambazo zinawakilisha Tabia au Mapenzi ya Mungu, hizi zipo wakati wote ambao Mungu yupo, pia kuna sheria zingine nyingi ambazo Mungu alizitoa zikilenga kifo cha Yesu. Mfano; Sheria za Kafara, Tohara, na maadhimisho mengine yaliyoambatana na sikukuu za upatanisho, pia kulikuwa na sheria ja kijamii – Mtu akizini apigwe mawe hadi kufa, ili waiogope zinaa n.k. Sheria hizo zote ziliisha baada ya wokovu kamili kukamilika kupiti kifo cha Yesu msalabani. Kwa ufafanuzi zaidi soma somo linalosema “SHERIA ZILIZOISHIA MSALABANI”.

9.      Tunahesabiwa haki kwa matendo ya  Sheria au kwa Imani?
Biblia inasema tunahesabiwa haki kwa Imani, Wagalatia 3:26-27 “Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani, katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo”.  Yesu alisema wazi kuwa pasipo yeye hatuwezi kutenda mapenzi ya Mungu (Hatuwezi kushinda Dhambi/kushika Amri), maana yake ni hii, kwa kumwamini Yesu Kristo, yeye anatuapatia Roho mtakatifu ambaye anatuvisha tabia ya Mungu ya Upendo. Hivyo tabia ya Upendo (Maisha bila dhambi) inakuwa ni tabia yetu. Haki kwa matendo ya Sheria ni kujitahidi kushika Amri au Sheria za Mungu kwa nguvu zetu kama walivyokuwa Mayahudi. Wanadai sio wauaji huku Hasira, Chuki na Visasi vimejaa mioyoni mwao – Hizo ni tabia za Mwili au Ibilisi. Pia hatuhesabiwi haki tena kwa Tohara na Kuchinja wanyama wa Kafara, kwani Yesu Kristo alishatulipia Deni kwa damu ya thamani.
ZINGATIA:
Sheria au Amri za Mungu
 Hazimuokoi mwanadamu, zipo kama kioo kinachoonyesha uchafu, lakini kioo hakiwezi kutumika kusafisha uchafu, mpaka yatumike Maji.

Neema
 Ndiyo pekee inayoweza kutuokoa, tukisamehewa dhambi na kutusafisha udhalimu wote kwa damu ya Yesu Kristo, hatimaye kutupatia ushindi wa kuishi bila Mawaa mbele za mungu.

HILA ZA SHETANI:
Nabii yohana alionyeshwa mwisho wa vita kati ya Mungu na Shetani ikiwa ni juu ya Kanisa la Mungu linalotii Sheria za Mungu na Imani ya Yesu.  “JOKA akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye VITA juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao AMRI za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa YESU;  akasimama juu ya mchanga wa bahari“ Ufunuo 12:17. Yesu akasema “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu hao wazishikao AMRI za Mungu na IMANI ya Yesu” Ufunuo 14:12.
 
Vita kati ya Mungu na Shetani ni juu ya SHERIA ZA MUNGU, shetani anakataa kumtii Mungu akidai na yeye kuwa ni sawa na Mungu. Wakati wote anasimama kupinga Sheria za Mungu na kuwafanya wanadamu wote wasimtii Mungu, kwa kupotosha au kubadili Amri za Mungu.  Viongozi wengi wa Dini wamedanganywa na kuongozwa kujenga chuki juu ya Sheria za Mungu. Neno la Mungu linasema “Yeye asemaye, nimemjua, wala hazishiki Amri zake ni Mwongo, wala kweli haimo ndani yake” 1Yohana 2:4, “Wokovu umbali na wasio haki, kwa maana hawajifunzi AMRI zako” Zaburi 119:155.

UNAALIKWA KUJIUNGA NA KUNDI LITALOSIMAMA UPANDE WA MUNGU KATIKA VITA KUU ILIYO MBELE YETU, TUNAPOFUNGA HISTORIA YA DUNIA HII.

Ev: Eliezer Mwangosi

No comments:

Post a Comment