Wednesday, March 14, 2012

AMRI YA 6 - USIUE

Ujumbe  unatoka:  Kutoka 20:13
Usiue.
tAFAKARI:
Katika jamii yetu, dhambi ya kuua ni kati ya makosa ya jinai, ambayo karibu kila mtu anaichukia. Lakini, mara nyingi utasikia watu wakisema “Ningelikuwa na uwezo ningemmaliza” na wengine wanawaendea wenzao kwa mafundi (wanganga) ili kupoteza uhai wao. Yesu alisema, “Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawambieni, kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu …” Mathayo 5:21-22.  Mungu anaangalia kilicho moyoni juu ya mtu mwingine.

Tendo lolote au hali yoyote inayosababisha kutoa uhai wa mtu, au kuleta hasira na ugomvi kati ya watu ni Dhambi ya kuua. kwa mfano: Kuingilia ndoa ya mtu na kusababisha familia kuteseka, Kuzua uongo ili kuleta chuki kati ya watu, Kutoa mimba au kusaidia kutoa mimba, kuua au kutupata watoto wachanga, mawazo ya hasira, kulipa visasi  na chuki juu ya wengine, moyo wa kutosamehe wanaowakosea, vinyongo, Kudhuru afya ya mtu kwa kumpa sumu au kumwendea kwa waganga n.k. Yote hayo ni uuaji. Mungu anasema “Kila amchukiaye ndugu yake ni MUUAJI: nanyi mnajua ya kuwa kila muuaji hana uzima wa milele ….” 1Yohana 3:15. Je kuna mtu yeyote Unamchukia? hata ukimuona anakukera?  Hiyo Sio salama. Mwambie Yesu akupatie Moyo wa kusamehe na Kusahau.

Uharamia mwingine wa mauaji ni pale unapomfanya mtu mwingine afe kiroho, yaani kumfanya atende dhambi. Mungu anajali zaidi Uhai wa kiroho kuliko wa kimwili, kwani mwili huu ni wa kitambo, Yesu alisema “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na Roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na Roho pia katika Jehanamu” Mathayo 10:28,  “Mshahara wa dhambi ni mauti ….” Rumi 6:23. Swali kwa wasomaji; ni wangapi leo wanatuhumiwa kwa mauaji? Tafakari: Huyo unayemwita “My Sweet Heart” au “My Honey” bila kujali ni mchumba wako, nyumba ndogo, hawala n.k. unampenda kweli? Ni kweli hakuna DHAMBI (Mauti) inayoendelea kati yenu?. Mungu anatupenda, ndio maana anatuletea ujumbee huu ili TUPONE kabla Mlango wa Rehema haujafungwa.

NAWATAKIA SIKU NJEMA NA BARAKA ZA BWANA ZIWE JUU YENU.

Ev:  Eliezer Mwangosi.
0755808077 & 0652571733
Kwa masomo zaidi fungua mitandao ifuatayo: http://emwangosi.blogspot.com/ (Vijana) http://kayanafamilia.blogspot.com/ (Ndoa) http://matengenezo.blogspot.com/ (Ujumbe wa Matengenezo)

1 comment:

  1. Mungu akubariki, nimebarikiwa na somo hili. Ni kweli watu wengi tunajua kuzitamka amri za Mungu ila hatuzielewi

    ReplyDelete