Sunday, March 18, 2012

UJUMBE KWA WATUMISHI WA MUNGU


Ujumbe  unatoka:  ISAYA 56:10-11,
Walinzi wake ni vipofu, wote pia hawana MAARIFA; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kulia; huota ndoto, hulala usingizi. Naam, mbwa hao wana choyo sana, hawashibi kamwe; na ni WACHUNGAJI wasioweza kufahamu NENO; wote pia wamegeuka upande, wazifuate njia zao wenyewe, kila mmoja kwa faida yake, toka pande zote.
tAFAKARI:
Giza nene la Kiroho linazidi kuisonga dunia yetu kwa sababu ya viongozi wa dini, na watu wengi sana wataangamia siku ya mwisho kwa sababu ya kupotoshwa na viongozi. Neno linasema “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani wangu mimi; kwa kuwa umeisahau Sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahu watoto wako” Hosea 4:6. Kizazi chetu kiko kwenye hatari kubwa, kwani Shetani ametunga falsafa nyingi za uongo, juu ya kweli ya neno la Mungu.

Wapendwa! Amkeni pambazuko liko karibu, mnapoona Dini na Madhehebu mengi yakianzishwa huku kila mmoja akiwa na mafundisho tofauti na mengine yaliyo kinyume neno la Mungu; jueni unabii umetimia, ukibahatika kuufahamu ukweli, changamka amua kuufuata ukweli. Mungu anasema “Kwa maana wawaongozao watu hawa ndio wawakoseshao, na hao walioongozwa na watu hao wameangamia” Isaya 9:16. Hapa hakuna usalama, Wachungaji wasiojua kweli ya Mungu na Waumini wao wanaokubali chochote bila kuchunguza ukweli, wote wataangamia.

Ujumbe huu ni sauti ya Matengenezo kwa kila anayejiita Mtumishi, bila kujali cheo chake. Neno linasema; wachungaji wamekuwa ni sawa na Mbwa Bubu asiyebweka adui anapovamia zizi la kondoo, hebu jiulize – Inakuwaje Uovu unadumu kati ya waumini? Kama Mtumishi anazini na waumini, au ni mlevi, muuza madawa ya kulevya n.k. waumini watakuwaje? Tunaona, Kwa sababu ya Maslahi! wenye pesa makanisani na miskitini hawakemewi hata kama wanafanya Dhambi za wazi, Viongozi wamepofushwa macho kwa sababu ya Maslahi.

Ohoooo! Wapendwa; wakemeaji wa dhambi siku hizi wako wapi? Manabii na waonyaji, kama akina Isaya, yeremia, Hosea, Ezekiel n.k. wako wapi siku hizi? Mbona wote wamegeukia Injili ya UTAJIRI na Kujikusanyia watu wenye Pesa kwa ajili ya maslahi yao? Wakati wote wakifundisha Ujumbe laini, wakikazia - uponyaji, utajiri, Baraka, Kupanda mbegu, Zaka na sadaka, amani n.k. huku waumini wakidumu kwenye Dhambi na hatimaye kuingia kwenye maisha magumu zaidi ya walivyokuwa mwanzo. Katika historia ya Biblia hakuna Nabii wala Mtume aliyekuwa na Injili ya akijilimbikizia Mali za Dunia hii mbali na Kuonya na Kukemea dhambi.

Hebu jiulize: Je Ni kweli wewe umetumwa na unaongozwa na Mungu? Huo ulevi, Hiyo tamaa ya Ngono, huko kupenda Fedha na utajiri, Hiyo mipango unayoungana na Dini ya mashetani kupinga kweli ya Mungu, huo upendeleo kwa wenye Pesa na kudharau maskini, na hiyo nyumba ndogo, na huyo Bwana asiye mume wako, na hayo madawa ya kulevya na biashara haramu, na huo utapeli na udanganyifu, na huko kugombania madaraka na kufanya kampeni kama vyama vya siasa, hiyo michezo michafu ya kuchezea mabinti za watu, na hizo hirizi unazotumia kuvuta watu na kutenda miujiza ukihadaa roho za watu kwa jina la Upako, hizo hasira, chuki, visasi na Mambo yanayofanana na hayo; Unaamini yanatokana na Roho Mtakatifu? – Msidanganyike; Mungu anasema “Tokeni kwake (Shetani na Mpinga Kristo), enyi watu wangu, msishiriki Dhambi zake, wala msipokee mapigo yake” Ufunuo 18:4.

Mbwa mwitu wamevamia kundi, nani wa kusimama kupiga kelele, wakati utitili wa mafundisho potofu yaliyo kinyume na ukweli wa neno la Mungu yakiingia kanisani!  nani wa kutoa maonyo na kutengeneza? Neno linasema “Lihubiri NENO, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, KARIPIA, KEMEA, na KUONYA kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundsho yenye uzima … na kuzigeukia hadithi za Oungo” 2Timotheo 4:2-4. Neema imefunuliwa ili kutuweka HURU mbali na Dhambi, sio kuhalalisha dhambi, kama wengi wanavyodai, huku wakizidi kuzama katika matope ya Dhambi.

MUNGU ATUBARIKI SOTE TUNAPOENDELEA KUFANYA MATENGENEZO KABLA SAA MBAYA HAIJAFIKA.

Ev:  Eliezer Mwangosi.

1 comment: